Events

SERIKALI YAWAHAKIKISHA WALIPAKODI KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO KWA HAKI NA USAWA

Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), imewahakikishia walipakodi nchini kuwa itashughulikia malalamiko ya wafanyabiashara yanayohusiana na kodi kwa haki na usawa ili kuchochea ulipaji kodi kwa hiyari.

Hayo yameelezwa na Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Bw. Robert Manyama, alipokutana na wadau wa kodi jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, wakati akitambulisha malengo ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo, iliyoanza rasmi kutekeleza majukumu yake.

Alisema Taasisi hiyo imeundwa na Serikali, chini ya Wizara ya Fedha, ikiwa ni Taasisi huru itakayokuwa na jukumu la kutoa usuluhishi wa malalamiko baina ya walipa kodi na watozakodi (Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA) ili kupunguza malalamiko ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu ambayo yamekuwa ni kikwazo kwa ulipaji kodi wa hiyari.

‘‘Tunatoa uwanja huru wa mlipakodi kupata haki yake bila kuona kuwa anayetoa usuluhishi wa malalamiko yake ni yuleyule aliyesababisha kutokea kwa malalamiko, lakini pia nitoe wito kwa wafanyabiashara wajitahidi kutunza kumbukumbu za biashara kwa usahihi ili kupata suluhu kwa kuzingatia ukweli na haki’’, alisema Bw. Manyama.

Alisema haki inaambatana na wajibu hivyo wafanyabiashara ni vema kutekeleza wajibu wao wakati Taasisi ikiwa inashugulikia malalamiko yao kwa kutoa ushirikiano wakati wanapohitajika kutoa taarifa fulani ili kuwezesha mchakato kufanyika ndani ya muda uliowekwa.

Bw. Manyama, alisema kuwa Taasisi hiyo pia katika kuzuia malalamiko inaendelea kutambua matatizo yaliyo ndani ya mfumo wa kodi yanayosababisha migogoro na kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mapendekezo ili kufanyike marekebidho ndani ya mfumo wa kodi.

“Tutashughulikia malalamiko kama yalivyo ila nasisitiza tuwe wakweli tukiwa wakweli tutatatua malalamiko, na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kupita mikoani ili kuweza kuwafikia katika maeneo yao’,’ alisema Bw. Manyama.

Alisema kuwa Taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuwa hakuna namna itaingiliana na majukumu ya Taasisi nyingine ya Serikali na kuwa Sheria iliyounda TOST imeipa uhuru wa kutokuingiliwa na Taasisi nyingine kiutendaji.

Naye Meneja wa Usajili wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bi. Naomi Mwaipola alisema kuwa maoni yaliyotolewa na wadau kuhusu kushirikiana ili kuwa na Taasisi imara yatafanyiwa kazi ili kuwa na mazingira yatakayochochea ulipaji wa kodi kwa hiyari.

‘‘Nawapongeza kwa michango yenu mliyotoa katika kikao hiki na tunaahidi kuwa itafanyiwa kazi na watumishi watatenda kazi kwa uadilifu ili kujenga imani ya wadau kwa Taasisi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla’’, alisema Bi Mwaipola.

Aliongeza kuwa Taasisi hiyo iko tayari kupokea malalamiko pamoja na maoni na kutoa rai kwa walipakodi kuanza kutumia huduma za Taasisi hiyo na kuwa itawafikia walipakodi katika mikoa yote.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Bw. Hamisi Livembe, aliipongeza Serikali kwa kuanzisha Taasisi hiyo na kutoa rai ianzishe ofisi mikoani ili kuweza kuwafikia wafanyabiashara wengi wa kati ambao wako mikoani ili changamoto zao za kikodi ziweze kushughulikiwa kikamilifu.

‘‘Waliopewa dhamana wawe na dhamira ya dhati kufanya kazi hiyo kwani ni kazi ngumu na waongeze uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kulinda haki za walipakodi’’, alisema Bw. Livembe.

TOST imekutana na wawakilishi wa wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wasafirisha Mizigo Tanzania (TAFFA), Jumuiya ya Walipakodi pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya kodi.