Chama cha Walipa Kodi Tanzania, TATA ni asasi huru isiyoegemea upande wowote iliyoanzishwa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kutetea mfumo wa kodi unaozingatia usawa, sheria na haki, kulinda haki za walipa kodi, na kutoa taarifa kamili kuhusiana na masuala ya mapato ya serikali yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi na matumizi ya kawaida na ya maendeleo.
TATA ni sauti ya walipa kodi nchini ambayo inataka sio tu kuwapa taarifa juu ya haki na uhuru wao lakini pia inafanya kazi ya kupeleka ujumbe kwa watunga sera, wafanya maamuzi, wakusanya kodi na jamii nzima kwa nia ya kuleta mabadiliko ya kimazingira na kitaasisi kuelekea mfumo huru na wa haki wa kulipa kodi nchini.
Ni wazi kuwa huduma kwa umma hazileti mkondo wa mapato ambao unaweza kgharamia huduma mbalimbali za umma. Kwa msingi huo, uboreshwaji wa uwezo wa sekta ya umma ili kuweza kuwa na matokeo mazuri itahitaji kuboresha ufanisi na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma, vile vile mapato makubwa ya serikali yatokanayo kodi.
Kwa bahati mbaya watu wachache wanawajibika katika ulipaji wa kodi kutokana na kutokuaminika kwa taasisi za umma na ukosefu mkubwa wa uzoefu wa jinsi ya kulipa kodi kwa hiari. Vilevile, watu wengi na wafanyabiashara wana uelewa kidogo kuhusu haki na wajibu wao na wa kusimamia kodi na hawaoni uwiano wowote kati ya mapato \ na matumizi ya serikali.