Historia
HISTORIA YA CHAMA CHA WALIPAKODI
Chama cha Walipakodi Tanzania (TATA) ni asasi huru ya kiraia, isiyoegemea upande wowote, ilianzishwa mwaka 1997 na kusajiliwa rasmi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 07, 1999. Asasi hii imeanzishwa kwa lengo la kuwaunganisha walipakodi na kupaza sauti zao katika kusimamia masuala yao na kuchochea mabadiliko hapa nchini.
Chama hiki ni miongoni mwa wanachama wa chama cha walipakodi Duniani (WTA) ambacho hulinda na kuunganisha walipakodi ili kushirikishana mbinu bora na kuunda fursa za ushirikiano pamoja na kueneza uhuru wa kiuchumi kwa mamilioni ya raia (walipakodi) ulimwenguni kote.
TATA ilitokana na hitaji la uwajibikaji wa serikali katika ukusanyaji na matumizi bora ya kod. Msukumo wa mpango huu ulikuwa ni mfadhaiko unaoongezeka kila mara miongoni mwa walipakodi kuhusu ongezeko la viwango vya kodi, matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za walipakodi katika matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya jamii na uchumi.
Kutokana na ukweli kwamba maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Taifa yanategemea mapato ya serikali yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi, kwa msingi huo walipakodi wanapaswa kutaka kuona kodi zao zinatumika ipasavyo na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa jamii unaozingatia thamani ya fedha na utimilifu wa haki zao za msingi za kibinadamu. Ni kutokana na hali hiyo TATA ilianzishwa ili kuunganisha sauti zao, katika kutetea haki, kusuluhisha migogoro ya kikodi, pamoja na kuhamasisha serikali kuwajibika katika ukusanyaji wa mapato kwa namna ambayo ni rafiki na kuhakikisha mapato hayo yanatumika kwa ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa umma, na kuzingatia thamani ya fedha na kuhakikisha uamuzi wa matumizi unakuwa wazi, pia kuhakikisha kuwa sheria na sera za kodi ni za haki, rafiki na zinazoeleweka na kwamba mzigo wa kodi ni nafuu.
TATA pia inajitahidi kuwapatia walipakodi nyenzo ambazo zinasaidia kuongeza uelewa kuhusiana na masuala ya kodi kuanzia ngazi ya chini na kupitia mitandao na kuleta maono yao serikalini kwa manufaa ya Taifa. Chama kinaendesha shughuli zake kupitia tovuti maalum, mitandao ya kijamii, na vyombo vya habari, pia, chama huandaa program maalum za kuwafikia walipakodi kupitia warsha na semina mbalimbali, vipidi redioni na televisheni, majukwaa ya walipakodi, kufanya tafiti, kuandaa majarida yenye lengo la kutoa elimu ya kodi na kutoa mapendekezo ya mabadliko na marekebisho ya sheria na sera za kodi kwa serikali na mamlaka za Mapato nchini.
Chama kilifanikiwa kushiriki vipindi mbalimbali vya uhamasishaji wa kodi kwenye vipindi maalumu kupitia Televisheni mfano “Malumbano ya Hoja” kinachorushwa na ITV na vingine vingi. Vile vile kupitia ziara kukusanya maoni ya walipakodi na kuwasilisha serikalini mapendekezo mbalimbali ya marekebisho ya sheria na sera za kodi, ambayo yalileta mabadiliko na uwezo wa kumudu walipakodi kabla ya chama kusitisha utendakazi wake mwaka 2015. Hata hivyo, bado kuna haja ya juhudi zaidi kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa kodi nchini Tanzania, ambayo yanaweza kupatikana ikiwa tutaungana kupitia TATA. Kupitia ustadi wetu wa ushawishi, kutumia vyombo vya habari, utaalamu wa watunga sera na sheria za kodi, tutahakikisha masuluhisho ya matatizo ya walipakodi yanapatikana kwa vitendo na njia rafiki.
Kuhamasisha uzingatiaji wa haki za walipakodi kote nchini, kupendekeza mabadiliko ya sheria na kanuni za kodi zisizo rafiki, au kero ambazo ni mzigo kwa walipakodi,na kuhimiza uwekezaji na ubunifu utakaowezesha kupanua wigo wa kodi, pamoja na kujenga biashara huria pia kuhakikisha ukuaji wa uchumi na kukuza mfumo huru na wa haki katika usimamizi wa kodi. Maelfu ya washawishi hufanya kazi kwa maslahi maalum na ya kibinafsi, lakini TATA ni "Mtetezi wa Walipakodi" Tunapambana ili kuhakikisha kwamba walipakodi wote (wadogo kabisa, wadogo, wa kati na wakubwa), wanakuwa na uwezo wa kufikia ndoto zao bila kuwa na mzigo mzito wa kodi unaowarudisha nyuma.
Tuungane kuleta mabadiliko. Mlipakodi, ndiye Mjenga Nchi.