Mamlaka ya Mapato Tanzania imesitisha ukamataji holela katika Soko la Kariakoo na maeneo mengine nchini, pamoja na kusitisha ufuatiliaji wa risiti za kielektroniki (efds) hadi Agosti, 2024.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amesema wanaendelea na utekelezaji wa maagizo yaliyowekwa na Serikali wakati wa kikao cha wadau cha kujadili na kutafuta suluhu ya migogoro ya wafanyabiashara kariakoo na mikoani. Katika kikao chake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam tarehe 15/07/2024
Mwenda amesema , hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za mashine za kielektoniki (EFD), kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi, kuweka mfumo wa utoaji nyaraka za manunuzi wakati wa uagizaji bidhaa, kubainisha na kusimamia orodha ya bidhaa nane kuwa na bei elekezi, kukamilisha maboresho ya mfumo wa Tancis na wataalamu wa forodha kukutana na Jumuiya za wafanyabiashara nchini ili kujadiliana taratibu za kiforodha,
Katika utekelezaji wa hatua hizo Kamishna amesema, Mamlaka ya Mapato Tanzania imejipanga kuongeza juhudi katika utoaji elimu kwa walipakodi na umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo semina za mabadiliko ya sheria za kodi, Elimu ya mlango kwa mlango, kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo makundi ya Whatsup pamoja na jumbe mbalimbali za kuelimisha, kutumia matangazo ya magari na vipeperushi mbalimbali na Vikao vya wadau wa kodi. Pia kurusha Matangazo kwenye TV, Radio, Magazeti na kutumia wasanii au watu mashuhuri.
Amesema, mifumo miwili ya kutoa nyaraka za manunuzi na wa bei elekezi eneo la forodha umekamilika tangu Julai 3, mwaka huu hivyo, kila mfanyabiashara atapata taarifa za kiforodha, pia ataweza kulipa kodi moja kwa moja bila kupitia kwa mfungashaji na kwamba ataelewa ni kodi gani inapaswa kulipwa.
Amesema kukamilika kwa Mfumo huo utasaidia kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata nyaraka zake za kiforodha na pia ataweza kulipia kodi moja kwa moja bila ya kupitia kwa mfungashaji wa mizigo yaani (Consolidator).
Amesema, katika suala la Kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo ni vitenge,Mashati,nguo nyingine,vipodozi,Vito vya thamani,nguo za ndani,leso na vesti zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika magari kazi hiyo tayari imeshafanyika na orodha ya bidhaa hizo nane tayari zimeshawekwa kwenye Tovuti ya TRA zikionyesha aina ya bidhaa, aina ya malighafi, vipimo vyake, bei ya bidhaa na kodi ya bidhaa husika.
Mwenda amesema maboresho ya TANCIS yakijumuisha mfumo wa Auto valuation yanaendelea na kwa sasa yapo kwenye hatua za utengenezaji wa mfumo na Maboresho hayo yatakamilika kufikia mwezi Januari, 2025 kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Pia, amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania inawafanyakazi wazuri na itaendelea kuwajengea uwezo, pamoja na kuwaadhibu wale ambao sio waadilifu.