Rais Samia amteua Balozi Sefue kuwa Mwenyekiti wa tume ya ushauri wa Kodi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemteua Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu kiongozi Julai 31, 2024, Balozi Dkt Moses Kusiluka imesema kuwa Rais Samia pia ameteua wajumbe nane wa tume hiyo ambao ni pamoja na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, (BOT) na Profesa Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Florens Luoga.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali mstaafu ambaye pia ni Profesa mstaafu wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Profesa Mussa Juma Assad nae ameteuliwa kuwa mjumbe wa tume hiyo.
Wajumbe wengine ni pamoja na aliyekuwa mtendaji mkuu wa Pricewaterhousecooper, Leornard Mususa, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Zanzibar,(ZU), CPA Aboubakar Mohamed Aboubakar na Mshauri wa masuala ya sheria Balozi Mwanaidi Maajar.
Wengine ni Mtaalamu na mshauri wa masuala ya kodi na aliyekuwa mkuu wa idara ya ushauri wa kodi, (PwC), David Tarimo, Katibu mkuu mstaafu, Balozi Maimuna Kibenga na Kamishna wa fedha za nje kutoka wizara ya fedha na aliyekuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania, (TRA), Rished Bade.
Kabla ya uteuzi huu, Rais Samia alitangaza uamuzi wa serikali kuunda kamati ya kutathmini na kushauri kuhusu masuala ya kodi mnamo Julai 29, 2024 wakati wa mkutano wa 15 wa baraza la taifa la biashara, (TNBC).
Mwisho