TRA yakusanya Tsh. trilioni 2.34 mwezi Julai
Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA) imekusanya jumla ya shilingi trilioni 2.246 sawa na asilimia 104.4 ya lengo lake la kukusanya shilingi trilioni 2.34 katika kipindi cha mwezi Julai, mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Taarifa ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda imesema kuwa makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 20.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.94 zilizokusanywa mwezi Julai kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2023/2024.
“Ufanisi katika makusanyo na ukuaji kwa mwezi Julai mwaka huu ni wa juu kabisa kufikiwa na Mamlaka katika kipindi cha miaka sita iliyopita” amesema Kamishna mkuu wa TRA katika taarifa yake.
Aidha Mwenda amesema ufanisi huu ni kiashiria chanya katika kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 la shilingi trilioni 30.4 linafikiwa.
Katika kuhakikisha hilo menejimenti ya TRA imejipanga kutekeleza kikamilifu mambo kadhaa ikiwemo kuimarisha mahusiano na ushirikiano na walipa kodi pamoja na wananchi wote, kutatuta changamoto za walipakodi, kushirikiana na Tume ya Raisi ya tathmini ya mfumo wa kodi nchini ili kuwa na mfumo rafiki, kusimamia utekelezaji wa makubaliano baina ya serikali na wafanyabiahsra pamoja na kusimamia uadilifu wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kufuatia ufanisi huu uongozi wa Chama cha Walipakodi Tanzania, kupitia Mwenyekiti wake Bw. Otieno Igogo unawapongeza walipakodi wote kwa kuendelea kulipakodi na kuahidi kuwa chama kitaendelea kuwa kipaza sauti chao katika kuhakikisha mfumo wa kodi unakuwa nafuu na rafiki.
Mwisho